Habari
Wadau wa Sekta ya Maji Wasisitizwa Kushirikiana Kutatua Changamoto za Rasilimali za Maji
Wadau wa Sekta ya Maji nchini wametakiwa kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja katika kutafuta na kutekeleza suluhisho la changamoto mbalimbali zinazokabili usimamizi, uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji, Bw. Robert Sunday, wakati wa kikao cha wadau wa rasilimali za maji kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Maji, Jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji pamoja na namna wadau wanavyoweza kushirikiana katika kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inalindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kikao hicho kiliwakutanisha wadau kutoka wizara mbalimbali za kisekta, taasisi za Serikali, mashirika ya maendeleo, wataalamu wa sekta ya maji pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi. Ushiriki wa wadau hao umeelezwa kuwa ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati shirikishi ya kukabiliana na changamoto zinazoathiri upatikanaji na uendelevu wa rasilimali za maji nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Sunday amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa, zinatunzwa na kuendelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na maendeleo ya taifa. Amesema mafanikio yaliyopatikana katika eneo hilo yametokana na juhudi za pamoja za Serikali, wadau wa maendeleo, taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja katika kuzitatua, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa vyanzo vya maji, ongezeko la mahitaji ya maji kutokana na ukuaji wa idadi ya watu, maendeleo ya kiuchumi na shughuli mbalimbali za kijamii na uzalishaji.
“Hatua iliyofikiwa katika utunzaji, ulinzi na uendelezaji wa rasilimali za maji ni kubwa, lakini bado tunahitaji kuongeza kasi ya ushirikiano ili kuhakikisha tunakuwa na mifumo madhubuti ya kusimamia rasilimali hii muhimu,” amesema Bw. Sunday.
Ameeleza kuwa maji ni msingi wa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini, ikiwemo kilimo, nishati, viwanda, afya, mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Kutokana na umuhimu huo, amesema usimamizi wa rasilimali za maji unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti, mashirika ya maendeleo na wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa rasilimali za maji zina mchango mkubwa katika kufanikisha mipango mikubwa ya Serikali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, ambayo inalenga kujenga taifa lenye maendeleo endelevu na uchumi imara unaozingatia matumizi bora ya rasilimali zilizopo.
Amesema ili kufikia malengo hayo, jitihada za mdau mmoja mmoja haziwezi kuwa na matokeo makubwa kwa haraka, bali zinahitaji kuwepo kwa mfumo wa ushirikiano unaowezesha wadau wote kushirikiana katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia hatua mbalimbali zinazohusu rasilimali za maji.
Kwa upande wake, baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha majadiliano ya pamoja baina ya wadau ili kubaini changamoto zinazojitokeza mapema na kuweka mikakati ya kuzitatua. Wamesema ushirikiano huo utawezesha matumizi bora ya rasilimali zilizopo, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi na kuhakikisha huduma za maji zinaendelea kuwa endelevu.
Wadau hao pia wameainisha umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, kuzuia uharibifu wa mazingira na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za maji.
Kikao hicho kimekuwa sehemu ya jitihada za Wizara ya Maji kuendelea kujenga jukwaa la ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji nchini. Kupitia ushirikiano huo, Serikali inalenga kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kwa ufanisi, zinalindwa dhidi ya changamoto mbalimbali na zinaendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.

