Habari

Imewekwa: Jul, 19 2025

Waziri Aweso Amtaka Mkandarasi Manyoni Kufanya Kazi Usiku na Mchana

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemuagiza mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Manyoni kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Waziri Aweso amemtaka mkandarasi M/S Megha Engineering & Infrastructure Ltd kutoka India kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaongezeka.

“Hakuna sababu ya kuchelewa. Kinachotakiwa ni kuongeza nguvu kazi na kufanya kazi usiku na mchana ili kutimiza dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Manyoni kupata huduma ya majisafi na salama,” Mhe. Aweso amesema.

Waziri Aweso ameongeza kuwa ameshuhudia majaribio ya pampu katika kisima kilichopo eneo la Mitoo ya Chini ambapo maji yanapatikana kwa wingi, hivyo nguvu sasa zielekezwe katika kukamilisha hatua zote zilizobaki.

Aidha, Waziri Aweso amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kwa usimamizi madhubuti wa mradi huo, huku akisisitiza umuhimu wa wataalamu wa Wizara kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mikoa katika ngazi zote ili kufanikisha miradi ya maji kote nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri, ameeleza kuwa Wizara ya Maji haitakubali uzembe wa aina yoyote na kwamba ifikapo Septemba 2025, maji lazima yawe yameanza kuingia kwenye matenki ya maji katika miji ya Manyoni na Sikonge.

“Kulingana na hatua iliyofikiwa kwenye miradi ya miji ya Manyoni, Sikonge na Kaliua, tunasisitiza kuwa kufikia Septemba 2025 maji lazima yawe kwenye matenki. Tutahakikisha hilo linafanyika kwa nguvu zote,” amesema Mhandisi Mwajuma.

Mradi wa Maji wa Manyoni unagharimu Shilingi bilioni 29 na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 64,667 kutoka kata za Mkwese, Muhalala na Manyoni Mjini. Hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60.

Ziara hiyo ya Waziri Aweso katika miji ya Urambo, Kaliua na Sikonge, mkoani Tabora na Manyoni, mkoani Singida imelenga kujiridhisha na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 pamoja na kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa viwango stahiki na kukamilika kama ilivyopangwa.