Habari
Waziri Aweso Atangaza Mikakati ya Kuboresha Huduma ya Maji Nchini
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ameweka wazi mikakati kabambe ya kufika katika lengo la Sekta ya Maji nchini wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni, jijini Dodoma.
Akibainisha utekelezaji wa mikakati ya Wizara ya Maji, Waziri Aweso amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa majisafi, salama na ya uhakika kwa wananchi wote kwa kutumia mbinu za kisasa, kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi. Ameeleza kuwa ili kufikia hayo, Wizara ya Maji imejiwekea mkakati mahsusi ambao ameuwasilisha kwa kina Bungeni.
Aweso amesema Wizara ya Maji inaendelea kuimarisha upatikanaji wa vyanzo mbadala vya fedha ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kupunguza utegemezi kwa bajeti ya Serikali. Alifafanua kuwa maandalizi ya Hati Fungani ya Sekta ya Maji (Water Bond) yanaendelea, ambayo italenga kuvutia fedha kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Hatuwezi kufikia malengo bila kuwa na fedha za kutosha. Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kupata vyanzo mbadala vya fedha ili kutimiza lengo la Serikali la kuwafikishia wananchi huduma bora na endelevu ya maji,” Aweso amesema.
Kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi, amesema Dira 2050 inaelekeza asilimia 70 ya fedha za uwekezaji zitoke sekta binafsi. Ameongeza kuwa Sera ya Maji ya Taifa ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025) imefungua milango kwa sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali na washirika wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Maji.
Aweso amesema Wizara ya Maji itaimarisha Mfuko wa Taifa wa Maji ili uweze kutoa fedha zaidi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, kuendeleza vyanzo vya maji na kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma bora. “Kupitia Mfuko huo, Wizara inaandaa Hati Fungani maalum ya Sekta ya Maji inayolenga kuvutia rasilimali fedha kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje, taasisi za fedha, mifuko ya hifadhi ya jamii na wawekezaji binafsi,” alifafanua.
Kwa upande wa teknolojia, amesema Wizara ya Maji itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma. Hii ni pamoja na mifumo ya kusoma mita kidijitali na maombi ya maunganisho ya maji mtandaoni. Amesisitiza ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla (Mita Janja) na kutangaza mkakati wa kuharakisha ufungaji wake kati ya mwaka 2026 hadi 2030.
Amebainisha kuwa hadi Aprili 2026, jumla ya Dira 23,156 zimefungwa vijijini na mijini ikilinganishwa na dira 13,526 mwaka 2025, lengo likiwa ni kufunga dira 1,114,133 kwa wateja wa mijini ifikapo mwaka 2030. Ameongeza kuwa changamoto ya ankara zisizo sahihi na utafutaji wa mivujo ya maji kwa macho zimepitwa na wakati.
“Mita Janja ndiyo suluhisho. Hakutakuwa na ukataji maji siku za mwisho wa wiki au sikukuu, na mteja atapewa taarifa kabla ya kukatiwa huduma,” Aweso amesisitiza. Aidha, ameelekeza kuwa wateja wote waliokatiwa maji au wenye adhabu mbalimbali wafike katika Mamlaka za Maji ili wapewe utaratibu wa kurejeshewa huduma.
Aweso amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta mbalimbali zinazotumia rasilimali ya maji ili kutekeleza miradi kwa pamoja. “Hatuhitaji kila sekta kujenga bwawa lake. Badala yake, tujenge mabwawa ya matumizi mbalimbali. Kwa ushirikiano huo, tutaendeleza pia uvunaji wa maji ya mvua kupitia mapaa na mabwawa,” alisema.
Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji inaakisi dhamira ya Serikali ya kuleta mageuzi ya kimsingi katika Sekta ya Maji kupitia ubunifu, ushirikiano wa kimkakati na matumizi bora ya teknolojia. Mikakati hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama nchini na kutoa mchango mkubwa katika kufikia maendeleo endelevu kama inavyoelekezwa katika Dira 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Waziri Aweso ameomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 1.120,194,614,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2026/2027. Kati ya fedha hizo, Shilingi 80,652,044,000 ni za matumizi ya kawaida na Shilingi 1,039,542,570,000 ni za maendeleo.

