Habari

Imewekwa: Sep, 30 2021

Mhandisi Sanga ataka Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu kuwa Endelevu

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amemtaka Mhandisi Mshauri kuzingatia uendelevu katika utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mkoani Simiyu (Simiyu Climate Resilience Project) katika kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji wa mradi kilichohusisha wataalam wa Wizara ya Maji, uongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wote watakaohusika na utekelezaji wa mradi.

Mhandisi Sanga amesema mradi huo wa kimkakati ni miongoni mwa miradi mikubwa mitatu inayotekelezwa na Serikali katika Sekta ya Maji utatekelezwa kwa gharama ya takribani Sh. bilioni 440 zitakazotoka kwa Shirika la Green Climate Fund (GCF), Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Serikali ya Tanzania, ambapo mkataba wa kuanza rasmi utekelezaji unatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.

“Mradi huu wenye awamu mbili za utekelezaji, awamu ya kwanza ikianza na wilaya za Busega, Itilima na Bariadi, awamu ya pili katika wilaya za Maswa na Meatu ni lazima uzingatie mpango wa muda mrefu kutokana changamoto ya hali ya ukame katika mkoa wa Simiyu, utekelezaji wake uhakikishe huduma ya uhakika kwa wananchi wote mkoani humo na nafasi ya kuongeza uwezo wa kufika maeneo mengi zaidi miaka ijayo.” amesema Katibu Mkuu Sanga.

“Kwa kuzingatia vigezo vya uendelevu wa mradi tumerudia usanifu wake na kuboresha baadhi ya vipengele vya kazi ikiwemo kuongeza uwezo wa chanzo kutoka lita milioni 20 mpaka milioni 54, kuongeza uwezo wa miundombinu hususan matenki ya maji na uwezo wa kutosheleza mahitaji kwa wananchi mpaka mwaka 2035 kwa lengo la kupata matokeo makubwa zaidi.” amesisitiza Mhandisi Sanga.

Mradi huu wenye lengo la kuleta maendeleo ya kiuchumi mkoani Simiyu unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 4 (Julai 2021-Agosti 2025) na kunufaisha wakazi wapatao 495,000 kwenye maeneo ya usambazaji wa huduma ya majisafi na salama, usafi wa mazingira, kilimo cha umwagiliaji na mifugo, lengo likiwa ni kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.