Habari
Mhandisi Mahundi aelekeza fedha za miradi ya maji zitumike kwa wakati

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameelekeza watendaji wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatumia kwa wakati fedha wanazopokea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Ameyasema hayo katika ziara ya kikazi wilayani Kisarawe baada ya kubaini kuwa zaidi ya shilingi milioni 100 hazijatumika katika kutekeleza mradi wa maji wa bwawa la maji la Chole wilayani hapo.
“Hili jambo tumeongea kwa muda mrefu kuwa fedha zinazoingia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zitumike kwa wakati. Mvua zimeisha muda mrefu. Wewe bado una zaidi ya shilingi milioni 100 kwenye akaunti wakati wananchi hawajapata huduma ya majisafi na salama. Hili halivumiliki.” Mhandisi Maryprisca amesema.
Ameongeza kuwa serikali inatoa fedha kidogo kidogo kulingana na hatua ya utekelezaji wa miradi na haiwezi kupeleka fedha katika maeneo ambayo bado kuna fedha ambazo hazijafanyiwa kazi.
“Lazima fedha itumike kwanza, tuone nini kimepungua ndipo tunapeleka fedha nyingine. Nasisitiza na kuwaagiza watekelezaji wa miradi kote nchini. Hakikisheni mnatekeleza miradi kwa wakati.”
Pia, amewaasa wataalamu wa Wizara ya Maji kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA, wilaya ya Kisarawe Mhandisi Majid Mtili ameeleza kuwa RUWASA imejipanga kufikisha majisafi na salama vijijini ili kupunguza kero ya upungufu wa huduma ya majisafi na salama.
Amesema mradi wa maji wa Chole utekelezaji wake ulisimama tangu mwezi Aprili kutokana na mvua nyingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Saimon amesema serikali inatambua changamotro ya upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya hiyo na kwamba itahakikisha inatatuliwa.
Amesema kwa sasa kiwango cha upatikananji wa maji kwa vijiji vya wilaya ya Kisarawe ni asilimia 65 na kwamba mpango uliopo ni kuongeza huduma hiyo hadi kufikia malengo yaliyoainishwa ya asilimia 85.