Habari

Imewekwa: Dec, 07 2021

Mabonde Watakiwa Kukabiliana na Changamoto ya Mabadiliko ya Tabianchi

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amezitaka Bodi za Maji za Mabonde nchini kuwa na mikakati mahsusi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ili kuzuia athari zake ikiwemo athari katika vyanzo vya maji.

Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo katika hafla fupi ya kusaini makubaliano ya utendaji baina ya Wizara ya Maji na Bodi za Maji za Mabonde kwa mwaka 2021/22 katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji, Mji wa Serikali jijijni Dodoma.

Lengo la makubaliano hayo ni kuongeza ufanisi wa mabonde tisa ya maji yaliyopo nchini.

“Tumeona athari za mabadiliko ya tabianchi zilivyoathiri maeneo mbalimbali nchini mwaka huu hadi kusababisha upungufu wa maji kwenye vyanzo vingi vya maji. Ili kuepuka hali ya aina hii isijirudie, Bodi zote za Mabonde zifanye tathmini ya kina kuhusu changamoto zilizotokea na kuweka mikakati mahsusi ili kukabiliana na athari zote zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Tuhakikishe mvua zinazonyesha zinakuwa na manufaa kwa kujenga mabwawa kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya baadaye na hasa katika kipindi cha ukame,” Mhandisi Sanga ameelekeza kwa watendaji wote wa Sekta ya Maji katika mabonde.

Pia, Mhandisi Sanga amezipongeza bodi hizo kwa kuongeza kiwango cha ufanisi kutoka asilimia 51 mwaka 2019/2020 hadi kufika asilimia 75.2 kwa mwaka 2020/2021 na kuzitaka kuongeza msukumo katika ukaguzi wa vibali vya maji vinavyotolewa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya maji kwa wateja wote mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha matumizi yake yanaendana na kibali kilichotolewa kisheria wakati wote kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo sahihi yanayoleta changamoto kwenye vyanzo vingi vya maji.

Awali, akiongea katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka Maafisa Maji wote wa Bodi za Maji za Mabonde kuwa mabalozi wazuri kwa kuwasaidia viongozi wa Wizara na Serikali kwa ujumla kusimamia vizuri na kutatua changamoto zote kwenye mabonde ya maji kwa kuwa maji ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, Mwenyekiti wa Maafisa Maji wa Bodi za Maji za Mabonde nchini, ambaye pia ni Afisa Maji wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani, Bw. Segule Segule amesema watahakikisha wanatimiza malengo yote waliyowekewa kwa ufanisi ili rasilimali za maji ziwe chachu ya maendeleo ya taifa.