Habari

Imewekwa: Nov, 06 2020

Maafisa Mawasiliano Sekta ya Maji Watakiwa kuwa Wabunifu katika Kuuhabarisha Umma

News Images

Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji nchini wametakiwa kuwa wabunifu wanapotekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanauhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipokuwa akifunga kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichomalizika leo mkoani Singida.

“Ninatoa wito, muwe wabunifu, mwende na wakati, muandike makala katika vyombo vya habari na majarida na mutangazeWizara kwa umma ikiwa katika taswira chanya” Mhandisi Kemikimba amefafanua.

Mhandisi Kemikimba amewaasa Maafisa hao kutobweteka kwa kusubiria vyombo vya habari vitangaze kuhusu sekta hiyo kisha waanze kujibu hoja zilizotolewa na badala yake wahakikishe wanauhabarisha umma kwa wakati kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 inayowataka kutoa habari kwa wananchi.

Aidha, Mhandisi Kemikimba amewaagiza Maafisa Mawasiliano hao kuhakikisha wanaifahamu vyema sekta nzima ya maji kwa ukamillifu ili kutekeleza ipasavyo jukumu la kuitangaza vizuri taswira ya Sekta ya Maji.

Mhandisi Kemikimba alihitimisha kwa kuwataka Maafisa Mawasiliano kujitathmini kwa kuangalia endapo katika maeneo yao ya kazi wananchi wanapata huduma ya maji nakuangalia miradi inayotekelezwa katika maeneo hayo endapo inafanya kazi na kushauriana na watendaji wao namna bora ya kuitangaza miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko, Chuo cha Maji, Bi. Ghanima Chanzi amesema kikao kazi hicho kitamsaidia kuboresha utendaji kazi.

“Ujuzi huu utaniwezesha kuhakikisha jamii inatambua chuo cha Maji kinafanya majukumu gani ya msingi katika Sekta ya maji mathalani katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya maji” Bi. Ghanima amesema.

Lengo la kikao hicho pamoja na masuala mengine ni kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi pamoja na kupata mafunzo juu ya masuala muhimu yanayohusu wajibu wa Maafisa Mawasiliano, Matumizi ya Mitandao ya kama njia ya Mawasiliano, Itifaki, Anuai za Jamii na umuhimu wa rasilimali za maji.

Kitengo cha Mawasiliano