Habari

Imewekwa: Sep, 15 2021

Katibu Mkuu Akutana na Ujumbe kutoka Taasisi ya Ushirikiano wa Maji Duniani (Global Water Partnership)

News Images

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amefanya mazungumzo kuhusu ushirikiano katika sekta ya maji hapa nchini na Ujumbe kutoka Taasisi ya Ushirikiano katika masuala ya Maji Duniani (Global Water Partnership, GWP)

Mhandisi Sanga amekutana na ujumbe huo ofisini kwake Dodoma, ukiongozwa na Katibu Mtendaji wa GWP, Kusini mwa Afrika Bw. Alex Simalabwi.

Mhandisi Sanga amewashukuru GWP kwa kutenga muda wao na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano uliopo baina ya Wizara ya Maji na Taasisi hiyo ambayo inashughulika na masuala ya maji katika nchi nyingi za Afrika na kuahidi kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano katika masuala yanayohusiana na maji kwa manufaa ya nchi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa GWP Bw. Simalabwi amesema kwamba lengo kubwa la kukutana na uongozi wa Wizara ya Maji ni kujitambulisha na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya (GWP) na Serikali.

Ameongeza kuwa jingine ni kuangalia namna ya kushirikiana katika maandalizi ya Kikao cha Viongozi wa Ngazi ya Juu Wanaoshughulika na Masuala ya Uwekezaji katika Maji unaotarajiwa kufanyika Zanzibar kuanzia tarehe 11 – 14 Disemba, 2021 na kumtambulisha rasmi Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo ya (GWP-SA) Rais Mstaafu Mh. Jakaya Mrisho Kikwete.

Amesema moja ya malengo makubwa ya (GWP) ni kukutanisha pamoja sekta mbalimbali zikiwemo Serikali, sekta binafsi na jamii katika kuunganisha nguvu ya kuweza kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya maji.

Wengine walioshiriki katika kikao hicho ni Katibu Mkuu Mstaafu Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye pia ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Bodi ya (GWP), Mhandisi Ngwisa Mpembe Mwenyekiti wa (GWP) Tanzania, Dkt. Victor Kongo, Mkurugenzi Mtendaji (GWP) Tanzania na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Maji.

Kitengo cha Mawasiliano