Habari
Kampuni ujenzi wa mradi wa majitaka Chato kuchunguzwa
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) ameelekeza Wizara ya Maji kuchunguza kampuni ya Peritus Exim PVT inayojenga bwawa la majitaka Chato.
Amesema uchunguzi huo uwe wa kina na hatua za kisheria zichukuliwe.
Amechukua hatua hiyo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa bwawa la majitaka katika mji wa Chato ambalo utekelezaji wake unasuasua tofauti na mkataba unavyoainisha.
Amesema bwawa hilo limepangwa kutekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5, na mkandarasi amelipwa zaidi ya shilingi milioni 800 lakini kazi iliyotekelezwa haiendani na makubaliano na haina viwango.
Pamoja na hilo, mkandarasi anatakiwa kuwepo eneo la kazi hata hivyo haonekani.
Mhe. Kundo amesema licha ya mradi wa Chato, mkandarasi huyo anayo miradi mingine katika mikoa mbalimbali ukiwemo Tabora ambako pia kumekuwa na malamiko.
Wakati huohuo Mhandisi Kundo amekagua mradi wa maji wa miji 28 mjini Chato na kuridhishwa na utekelezaji wake. Amesema mradi huo umefika asilimia 65, na unatarajia kukamilika Novemba 30, 2026 na kazi kubwa yenye ubora stahili inaonekana wazi. Amempongeza mkandarasi na wasimamizi wa mradi huo kwa ngazi zote kwa kuendelea kuiheshimisha sekta ya maji kwa kugusa mahitaji ya wananchi.
Amemuahidi Mbunge wa jimbo la Chato Kusini Mhe. Paschael Lutandula kuwa serikali itahakikisha mradi huo ambao kwa sasa unalenga kuhudumia kata nane za Chato mjini unaongezeka na kugusa maeno yote ya wilaya ya Chato ikiwemo jimbo la Chato Kusini. Amesema mradi huo ni sehemu ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo wao kama watekelezaji hawawezi kwenda kinyume.

