Habari

Imewekwa: May, 05 2021

Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji yaridhishwa na kasi ya utekelezaji miradi ya maji Dodoma

News Images

Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji imetembelea maeneo mbalimbali katika jiji la Dodoma na kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA) kuondoa changamoto ya upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa wakazi wa jiji la Dodoma.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Christine Ishengoma (Mb) amesema kamati imeridhishwa na jitihada zinazofanywa na serikali na kwamba matumaini ya kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji Katika jiji ziko wazi ndani ya muda mfupi.

“Niwapongeze viongozi wa Wizara ya Maji kwa jinsi mnavyohangaika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji. Sisi sote tunatambua kwamba baada ya Serikali kuhamia Dodoma, idadi ya watu iliongezeka na kusababisha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa kubwa lakini kwa jinsi mnavyokwenda, ni wazi tatizo hili linaweza kuisha hata ndani ya mwaka mmoja”. Amesema Dkt. Ishengoma.

Amesema Kamati inatambua kipindi kigumu wanachopitia wananchi wa jiji la Dodoma Katika kupata huduma ya majisafi lakini wasife moyo matumaini yapo na yanaonekana wazi.

"Tumeona visima mnavyochimba ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji. Hiyo ni hatua nzuri. Muendelee hivyohivyo."

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) amesema wanafanya kila jitihada kuhakikisha mji wa Dodoma unapata Maji na hivyo kuondoa kabisa changamoto hiyo.

"Niwahakikishie kuwa sisi Viongozi wa Wizara ya maji hatutakuwa kikwazo kuhakikisha wananchi wa Dodoma wanapata majisafi, salama na yenye kutosheleza." Amesema Mhe. Aweso

Kamati hiyo imetembelea maeno ya Mzakwe kwenye vyanzo vya maji yanayohudumia mji wa Dodoma na kushuhudia visima virefu bikivhimbwa pamoja na eneo la Chamwino kunakojengwa tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili na laki tano.