Habari

Imewekwa: May, 07 2020

EWURA yatakiwa Kudhibiti Changamoto za Sekta ya Maji

News Images


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetakiwa kuchukua hatua madhubuti zitakazotatua changamoto zote katika Sekta ya Maji kama chombo chenye mamlaka ya kusimamia huduma ya maji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) wakati akizungumza na Menejimenti ya EWURA akisisitiza mabadiliko ya kiutendaji kwa taasisi ndiyo yatakayotoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zilizopo na kuchangia sera ya Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Naibu Waziri Aweso amesema kumekuwa na malalamiko mengi kwa sasa hususani kwa upande wa huduma ya maji, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuhakikisha inafikisha huduma hiyo mijini na vijijini kwa kutumia fedha nyingi kwenye ujenzi wa miradi ya majisafi na majitaka.

Akitolea mfano baadhi ya mamlaka kuchukua hatua ya kujipangia bei bila kuidhinishwa na EWURA kinyume na sheria. Pia, akiitaka iangalie upya gharama za maji vijijini zinazoonekana kuwa kubwa kuliko mijini licha ya tofauti ya kiuchumi iliyopo katika maeneo hayo.

Naibu Waziri Aweso ameilekeza EWURA ianze utaratibu wa ukaguzi wa dira za maji mara kwa mara kwa lengo la kufahamu ubora wake, namna zinavyofanya kazi na kusimamia zoezi zima la usomaji ili kudhibiti ankara za maji zisizo sahihi kwa wateja.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje amesema kwa sasa wameandaa mpango

wa utoaji elimu kwa mtoa huduma na mtumia maji itakayoelezea haki na wajibu wa kila mmoja itakayosaidia kupunguza tofauti zilizopo baina ya makundi hayo mawili.

Akifafanua kuwa miongoni kwa majukumu ya msingi ya EWURA ni kutoa miongozo na kanuni mbalimbali kuhusu utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, kupima na kusimamia ubora wa maji, pamoja na kuchambua na kuidhinisha bei za huduma za maji na usafi wa mazingira kwa mamlaka zote 68 za maji nchini.