Habari

Imewekwa: Mar, 16 2022

Dkt. Mpango Azindua Maadhimisho ya Wiki ya Maji na Kuweka Jiwe la Msingi Kwenye Mradi wa Maji Orkesumet

News Images

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametaka watu wote wanaokwamisha na kuhujumu miradi ya maji kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Dkt. Mpango ametoa agizo hilo katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa katika hafla iliyofanyika katika Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kipaumbele kwenye Sekta ya Maji kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji na haitakuwa tayari kuona miradi hiyo ikikwamishwa au kuhujumiwa na mtu yeyote.

Akizitaka mamlaka husika kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia, kuitunza na kuilinda miradi hiyo pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote wenye tabia hiyo ili miradi hiyo iweze kudumu na kutoa huduma ya maji kwa muda mrefu.

Pia, Dkt. Mpango amesema kuwa ni muhimu kutunza mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuwa na vyanzo vingi na vya uhakika vya maji kwa kuwa ndio msingi wa huduma bora ya maji na ya uhakika wakati wote.

Dkt. Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa kuing’arisha Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa na nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Wizara hiyo ili kufikia lengo yake ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025.

Awali, Dkt. Mpango aliweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Maji wa Orkesumet wilayani Simanjiro wenye thamani ya Shilingi bilioni 41.5 utakaohudumia zaidi ya wakazi 52,000 na mifugo katika kata za Orkesumet, Langai na Edonyongijape na vijiji vya jirani na mji wa Simanjiro, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 99 chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) na kutoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Mhandisi Iddy Msuya kwa usimamizi mzuri.

Aidha, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kuwa kwa sasa hali ya utekelezaji wa miradi ya maji ni nzuri na kuwataka Wataalam wa Sekta ya Maji kuongeza ufanisi katika kusimamia, kuendesha na matengenezo ya miradi hiyo ili kuendelea kutoa huduma kwa miaka mingi ijayo.

Maadhimisho ya Wiki ya Maji huadhimishwa tarehe 16 – 22, Machi kila mwaka, ambapo Kilele cha Maadhimisho yake kwa mwaka huu yatafanyika Jijini Dar es Salaam na Mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.