Habari
Naibu Waziri Kundo Aongoza Ujumbe wa Tanzania Mkutano wa Mawaziri Wa Bonde la Ziwa Victoria Nchini Kenya

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) Jijini Kisumu, nchini Kenya.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), Mhandisi Kundo alisema mkutano huo umejikita katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya pamoja ndani ya Bonde la Ziwa Victoria, pamoja na kujadili mikakati ya upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi mipya ya maji na mazingira.
“Mkutano huu umetupatia fursa ya kutathmini mafanikio ya miradi inayoendelea kutekelezwa, hasa ile ya ushirikiano wa kikanda, sambamba na kupanga mikakati ya kupata rasilimali zaidi ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi wa ukanda huu,” aMhandisi Kundo amesema.
Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wakuu wa miradi ya LVBC, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya majitaka katika Jiji la Mwanza, na utekelezaji wa Mradi wa Kikanda wa Usalama na Uokoaji kwenye Ziwa Victoria.
Aidha, miradi mipya inayopendekezwa na kutafutiwa fedha inahusisha upanuzi wa huduma za majitaka katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa maendeleo endelevu.
Mkutano huo pia ulijadili kwa kina changamoto ya kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Victoria, ambapo Mawaziri kutoka nchi wanachama walikubaliana kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na tatizo hilo ambalo linaathiri shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayozunguka ziwa hilo. Sekretarieti ya LVBC imeagizwa kuandaa na kuwasilisha mpango mkakati wa haraka wa kutatua changamoto hiyo.
Mbali na Naibu Waziri wa Maji, ujumbe wa Tanzania pia ulihusisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb), pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb).
Baraza hilo la kisekta linajumuisha mawaziri kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na lina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kwa manufaa ya wananchi wa ukanda huo.