Habari

Imewekwa: Mar, 08 2023

​Chuo cha Maji chatakiwa kuwa maabara ya sekta ya maji

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amekitaka Chuo cha Maji kuwa maabara ya kutafiti na kutoa majibu kwa changamoto mbalimbali zinazotokea katika Sekta ya Maji hapa nchini.

Mhe. Aweso amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Kisayansi la Maji jijni Dar es salaam lililoandaliwa na Chuo cha Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Maji.

“Kongamano hili ni moja ya tukio la Wiki ya Maji hivyo kuweni maabara ya kutoa majibu katika sekta ya maji kwa sababu Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa hapa nchini” Mhe.Aweso amesema na kuongeza lengo la Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kumtua mama ndoo ya maji kichwani na kuleta maendeleo zaidi kwa jamii ya Watanzania.

Waziri Aweso amesema teknolojia na mazingira vinabadilika hivyo ni muhimu kubadilika na kwenda na wakati, na kusisitiza mabadiliko yanahitaji wataalamu zaidi katika kuendesha na kusimamia miradi ya maji.

Amesema kufanyika kwa kongamano kwa mara ya pili ni moja ya njia ya kubadilishana uzoefu na mbinu kutoka nchi mbalimbali ili kuimarisha huduma ya maji hapa nchini.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akiongea katika kongamano hilo amesema siku za usoni kongamano litaimarishwa zaidi kisekta, na lengo likiwa kuweka mikakati ya kufikisha na kuimarisha huduma ya maji katika jamii.

Mkuu wa Chuo Dkt. Adam Karia amesema washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanashiriki kongamano hilo la kimataifa linalofanyika kwa mara ya pili hapa nchini.

Kongamano la Kimataifa la Kisayansi la Maji ni moja ya matukio ya Wiki ya Maji 2023, ambayo ilianza kuadhimishwa hapa nchini mwaka 1988 ikiwa na matukio mbalimbali kuelekea Siku ya Maji Duniani Machi 22.

Kitengo cha Mawasiliano