Habari

Imewekwa: Oct, 30 2019

Bilioni 10.6 Kumaliza Tatizo la Maji Kisarawe

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Dar es Salaam: 30 Oktoba, 2019

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha Mradi wa Maji wa Kisarawe, mkoani Pwani unaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka kwa sababu asilimia 99 ya mradi huo umekamilika.

Naibu Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo mara baada ya kuukagua mradi huo na kutaka tenki la mradi huo lenye ujazo wa lita milioni 6 liwe limejaa maji ndani ya siku tatu kuanzia leo tayari kwa kufanyiwa majaribio.

Akisema hakuna sababu ya kuendelea kusubiri kwa kuwa mradi umeshakamilika kwa asilimia kubwa kinachotakiwa ni kumalizia kazi ndogo zilizobaki ikiwemo ujenzi wa vilula vya maji kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wakati kazi ya kuunganishia wananchi nyumba kwa nyumba ikiendelea.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso ameielekeza DAWASA ifikishe huduma ya maji katika Shule ya Sekondari ya Pugu na Shule ya Msingi Chanzige zilizopo wilayani Kisarawe kupitia mradi mkubwa wa Maji wa Kisarawe kwa lengo la kumaliza tatizo la maji kwa shule hizo ziweze kufanya vizuri zaidi kitaaluma na kuzalisha viongozi wa baadae.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji na Miradi DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema mradi huo wenye thamani ya Bilioni 10.6 uliojengwa kwa fedha za ndani za DAWASA utatoa maji kutoka Tenki la Maji la Kibamba hadi Kisarawe.

Akisema mpaka sasa kazi za ulazaji wa bomba kuu kilometa 17 kutoka Kibamba na mabomba ya usambazaji zaidi ya kilometa 34 kwa Mji wa Kisarawe zimekamilika, kazi iliyobaki ni kufunga umeme inayotegemewa kukamilika ndani ya siku mbili.

Utekelezaji wa mradi huo ni kutimiza agizo la Rais, Mhe. Dkt. John Magufuli la kupeleka maji Kisarawe kutoka Mtambo wa Ruvu Juu uliopo katikae Wilaya yaMlandizi, mkoani Pwani.