Habari

Imewekwa: Nov, 15 2023

​Benki ya Dunia yatoa heko kwa Tanzania kuhusu Miradi ya Maji ya Lipa kwa Matokeo

News Images

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Victoria Kwakwa ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza kwa ubora na viwango Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (PforR) na kuwa kinara wa nchi nyingine Duniani zaidi ya 50 zinazotekeleza programu hiyo.

Dkt. Kwakwa ametoa pongezi hiyo jijini Addis Ababa katika mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika unaohusu masuala ya upatikanaji wa majisafi na salama na usafi wa mazingira.

Ameitaka Tanzania kutoa uzoefu wa mafanikio yake kwa nchi zaidi ya 23 za Mashariki na Kusini mwa Afrika zinazoshiriki mkutano huo.

Programu hiyo inatekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo Tanzania ilipata Dola za Marekani milioni 350 katika miaka mitano na katika miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji ilikuwa imefikisha huduma ya maji kwa zaidi ya watu millioni 4.7 vijijini katika mikoa 17.

Kufuatia mafanikio hayo, na kulingana na matokeo , Benki ya Dunia iliongeza Dola za Marekani milioni 300 na hivyo kuongeza wigo wa utekelezaji na kufikia mikoa 25, hivi sasa shillingi milioni 970 zimepelekwa katika kila Halmashauri nchini Tanzania ili kuanza utekelezaji.

Mafanikio ya PforR yamefungua milango ya uendelevu wa programu hiyo ambayo itafikia ukomo Julai 2025. Hivyo, Kufuatia hoja ya Tanzania ya kuwa na PforR Awamu ya Pili, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kuwa na PforR Awamu ya Pili katika kipindi cha 2025-2030.

Programu ya PforR imewezesha Wizara ya Maji kufanikisha miradi ya maji 1,500 ambayo inatoa huduma kwa maefu ya wananchi.

Kitengo cha Mawasiliano