Habari

Imewekwa: Sep, 25 2022

Aweso awataka wananchi wasiamini ushirikina katika sayansi ya maji

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ((Mb) ametembelea mradi wa maji wa kijiji cha Wiyenzele Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma na kumuagiza Meneja waWakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Mpwapwa Mhandisi Cyprian Warioba kuhakikisha ndani ya siku 30 anatanzua changamoto kuhusu kukamilika kwa mradi huo.

Video ya tukio hili BofyaHAPA

Mhe. Aweso ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu mradi huo uliokamilika mwaka 2016, namwaka 2020 mradi huo ulipata changamoto ya kuharibika kwa pampu.

Wamesema matengenezo ya pampu hiyo yamekuwa yakifanyika kupitia wakandarasi tofauti tofauti bila mafanikio.

Baada ya matengenezo hayo kushindikana, pampu mpya ilinunuliwa lakini bado huduma haijarejeshwa.

"Niwaombe radhi wananchi. Tusitafute mchawi.Hawa wataalamu wetu ndio wanatakiwa kutumia maarifa yao kutekeleza mradi huu kwa kuzingatia hali ya udongo wa eneo hili.

Nawaagiza mbele yenu. Ndani ya mwezi mmoja changamoto zote za eneo hili zipatiwe ufumbuzi. Maji yaanze kutoka."Waziri Aweso amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibakwe ambako kijiji hicho kinapatikana Mhe. George Simbachawene (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu amewataka wananchi waiamini Serikali, waache kukimbilia imani za kishirikina badala yake wakae pamoja na wataalamu wa Wizara ya Maji, washirikiane na viongozi wa dini na wazee mashuhuri kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi.