Habari

Imewekwa: Sep, 10 2020

Ziwa Viktoria limefungua fursa za kiuchumi Tabora.

News Images

Katika maeneo mengi aliyogusia Mheshimiwa Rais wakati akilihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni suala la huduma ya majisafi na salama kwa watanzania. Aliweka wazi kwamba mwaka 2015 kiwango cha upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini ilikuwa asilimia 47. Hadi mwaka 2020 huduma hiyo imepanda hadi kufikia 70.1%. Aidha kwa upande wa mijini huduma hiyo imepanda kutoka 74% hadi 84%.

Eneo moja aliloliongelea kwamba limesaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha mafanikio hayo ni mradi wa kusafirisha maji kutoka ziwa Victoria hadi mkoani Tabora ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHWASA).

Hadi Februali mwaka huu taarifa ya Wizara ya Maji kuhusu utekelezaji wa mradi huo katika miji ya Nzega, Tabora, Igunga na Uyui, inaonesha kuwa miji yote hiyo pamoja na vijiji 92 vilivyoko maeneo hayo vimefikiwa na huduma ya majisafi wakativijiji kumi vikitarajiwa kufikiwa hivi karibuni.

Hili jambo siyo dogo kwa sababu maeneo hayo yamekuwa na hali ya ukame na upungufu wa majiambao umekuwa ukienda sambamba na ukosefu wa huduma ya majisafi na salama ya kutosheleza kwa saa zote, bila mgao. Hali hiyo imechangia kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wakazi na wananchi wengine. Magonjwa ya kuambukiza hasa yale yanayotokana na matumizi ya maji yasiyosalamayamekuwa yakitajwa sana katika maeneo haya. Malalamiko na mrejesho wa wananchi hao umeifikia serikali na kufanyiwa kazi.

Mafanikio ya upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika ni kuashiria safari mpya ya mafanikio katika nyanja zote za Maisha.

Kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo youtube yenye viunganishi https://www.youtube.com/watch?v=3mbOrDftDwg Pamoja na https://www.youtube.com/watch?v=0wG6iVJiIOk Wananchi wa miji hii wamesikika wakipaza sauti zao kuishukuru serikali kwa kusikia kilio chao.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora (mstaafu) Ndugu Aggrey Mwanri ambaye amekuwa akisikika mara nyingi kwa mipango ya kuifanya Tabora kuwa kama jiji la Toronto, kwa bara la Afrika anasema maji yameileta Toronto ya kweli aliyoihubiri kwa muda mrefu. Anaenda mbali kwa kueleza kwamba changamoto ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu ikiwemo homa ya matumbo na magonjwa ya kuhara imepungua sana mkoani Tabora mara baada ya mradi mpya kufikisha maji katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma.Zaidi, pamoja na hilo anawaalika wawekezaji kuelekeamkoani Tabora kwani changamoto kubwa za mkoa huo ikiwemo huduma ya maji Serikali imezitatua.

“Hakuna mwekezaji anayetamani kwenda kuwekeza katika eneo ambalo lina uhaba wa maji. Toronto ya kweli sasa imefika. Niwaombe Watanzania wote, wakiwemo wakazi wa Mkoa wa Tabora walioko ndani na nje ya nchi waje kuwekeza nyumbani”, Mhe. Mwanri anasema.

Bi. Pili Mweda ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga anasema walikuwa na kawaida ya kuchangia matumizi ya maji na mifugo wakati huo wakitegemea maji kutoka bwawa la Mwanzugi. Naye Edina Philipo Mkazi wa Igunga anasema iliwahi kutokea wakavamiwa na watu ambao walishindwa kuwatambua wakati wakienda kuchota maji nyakati za usiku.

“Mimi mwenyewe niliwahi kukimbizwa usiku nikifuata maji. Bahati nzuri nilikimbia nikapiga kelele aliyekuwa akinikimbiza akaniacha. Kwa kweli ujio wa maji haya umepunguza matatizo mengi ya kifamilia huku kwetu”.

Mathias John, Mkazi wa Ziba Kitongoji cha Igumila wilayani Nzega anasema uhaba wa maji ulikuwa umeleta utaratibu mpya wa maisha. Badala ya utaratibu wa kawaida wa maji kuchotwa na akina mama, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na akina baba kwa kutumia maguta, mikokoteni au baiskeli.

Akiongelea mabadiliko baada ya mradi mpya kuanza kazi, Elifuraha Keflasi Mpanda anayeishi Mtaa wa Mwayunge Wilayani Igunga ambaye anasema maji yamemfanya aione fursa mpya ya kilimo cha bustani ya Mbogamboga na ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya biashara.

“Nafurahi sasa nimeiona fursa mpya. Nafyatua matofali, nauza, nalima bustani na kuzalisha mbogamboga ambazo zinaniongezea kipato”.

Mbali na wananchi mkoani Tabora uongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wilayani Igunga ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Mhandisi Rafaeli Melumba anasema kabla ya mradi kuna wakati serikali ilikuwa inalazimika kuingia gharama kubwa kusomba maji kuwapelekea wananchi kwenye maeneo yao.

“Kwa mfano mwezi wa kumi mwaka jana tulilazimika kuingia gharama ya kusomba maji kuwapelekea wananchi kwenye maeneo yao kutokana na ukame uliosababisha kukauka kwa mabwawa yote likiwemo bwawa la Bulenya ambalo wamekuwa wakilitegemea.” Mhandisi Melumba anasema.

Vilio vyote hivi vinaonesha jinsi tatizo la maji lilivyokuwa kubwa katika maeneo hayo. Shida hiyo ilikuwa imezalisha utamaduni mpya wa maisha, ugumu wa maisha ulikuwa umebadilika kuwa hali halisi ya maisha ya Igunga. Sasa hali imebadilika. Ujio wa maji unafungua fursa nyingi za kiuchumi mkoani Tabora na kupunguza gharama za maisha kwa familia za wananchi.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Mzee Lumanila Kija wa Kijiji cha Ziba wilayani Nzega anasema gharama za maji zimepungua kutoka kati ya shillingi 500 hadi 1000 kwa ndoona kwa sasa kuwa shilingi 30 hadi 50 kwa ndoo. Mzee anasema kama sio umri wake, angekuwa bado ni kijana, angeweza kufanya makubwa kwa sababu alishindwa kufanya mengi wakati wake kutokana nasehemu kubwa ya maisha yake kutumia muda mwingi katikautafutaji wa maji kwa matumizi mbalimbali ya familia.

Maji yamefungua fursa mpya za kibiashara. Adamu John wa kijiji cha Ziba anasema ujio wa maji umemfanya aanze biashara ya kuchuuzamaji ambapo kwa sasa anawapelekea wananchi majumbani mwao hasa wale ambao hawana nafasi ya kufika kwenye vioski vilivyojengwa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa wananchi wote. Kazi hiyo imemuwezesha kununua baiskeli mpya na kuanza ujenzi wa nyumba ya kudumu.

Maji yameleta fursa ya kilimo cha biashara. Sadda Juma mkazi wa Nzega anasema sasa anaweza kulima mbogamboga kwa ajili ya chakula cha familia na ziada anayoipata anafanya biashara.

Agostino Petro Maridadi, Mkazi wa Mwanzugi Igunga anasema sasa ni mfanyabiashara wa tofali. Anafyatua, kuchoma na kuuza. Hilo limemsaidia kujikwamua kiuchumi na kukidhi mahitaji ya familia na kuwasaidia ndugu zake wengine katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Hili ni jambo kubwa na la faraja kwa wananchi. Ni jambo ambalo Serikeli yoyote inayojali maslahi ya umma italizingatia. Heri kwa wana-Igunga, Heri kwa Watanzania. Heri kwa Serikali ya awamu ya Tano. Ndoto ya kumtua mama ndoo imetimia na kazi inaendelea katika maeneo mengine kuwaletea huduma ya maji Watanzania.