Habari

Imewekwa: Jun, 03 2021

Wizara ya Maji yaanzisha Luku za maji

News Images

Wizara ya Maji imeanza rasmi mabadiliko kwa kuelekeza matumizi ya Dira za maji za malipo kabla (pre-paid meter) ili kuondosha malalamiko ya kuwepo kwa bili bambikizi, pia kuendana na maendeleo ya teknolojia.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya kilimo mifugo na Maji.

Amesema nia ya mabadiliko hayo ni kumaliza changamoto ya malalamiko ya wanachi kuhusu kusomewa Dira bila kushirikishwa huku akipiga marufuku watendaji wa sekta ya maji kuwakatia wanachi huduma ya maji wakati wa siku za sikuuu na siku za mapumziko.

“Ni marufuku kumkatia maji mwananchi siku ya sikukuu au mwishoni mwa wa wiki. Tulipoweka hii hatujaweka kama adhabu" Aweso amesema .

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema mfumo huo utaweza kudhibiti matumizi ya maji kwa kutumia simu ya mkononi kwa kununua maji sehemu yoyote na Dira kujifunga muda maji yakiisha na kujifungua mara baada tu ya kulipia huduma. Pamoja na hilo mteja anao uwezo wa kuhama na maji aliyoyanunua endapo akihama makazi.

“Unaweza ukakaa nyumba X lakini ukihamia nyumba Y unachukua zile unit zako unahama nazo", Mhandisi Sanga amesema.

Ameongeza kuwa Wizara ya Maji imefanya mazungumzo na kampuni zinazohusika na utengenezaji wa Dira hizo ili kujenga kiwanda hapa nchini.

Mhandisi Sanga amesema mfumo huo unamwezesha mteja akiwa safarini kuangalia kiasi cha maji kilichotumika katika Dira yake.