Habari
Wizara ya Maji kutoa Vibali vya Miradi ya Maji Sengerema

Mwanza; 05 Disemba, 2019
TAARIFA KWA UMMA
Wizara ya Maji imetangaza itatoa vibali kwa ajili ya kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Sima, Nyasigu, Lubungo na Ngoma katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa kauli hiyo akiwa ziarani katika Wilaya ya Sengerema akikagua miradi ya maji na kukuta kazi ya ujenzi wa miradi hiyo haijaanza kutokana na kukosekana kwa vibali.
Akawatoa hofu wakazi wa vijiji vya Sima, Nyasigu, Lubungo na Ngoma kuwa Serikali imeshatenga fedha za ujenzi wa mradi na kumuelekeza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wa vibali hivyo ili kazi hiyo ianze haraka.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso ameilekeza Wakala wa Usambazaji wa Maji Vijijini (RUWASA) kuukamilisha Mradi wa Maji wa Nyakalilo/Bukokwa katika Halmashauri ya Buchosa ambao una miaka mitano tangu utekelezaji wake uanze na haujakamilika.
Mhe. Aweso amesema haiwezekani mradi wa zaidi ya bilioni 1.3 uchukue miaka mitano bila kukamilika na kutochukua hatua zozote, hakuna haja ya kumsubiri mkandarasi na kuitaka RUWASA kuukamilisha mradi huu haraka.
Aidha, Kaimu Meneja wa RUWASA mkoa wa Mwanza, Mhandisi Warioba Sanya amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyorithiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema watajipanga kukamilisha mradi huo kwa kuwa Shilingi milioni 69 zilizobaki zinatosha kumaliza kazi.
Kitengo cha Mawasiliano