Habari

Imewekwa: Sep, 24 2021

Waziri Mkuu Ataka Mazungumzo yafanyike Wizara ya Maji na Mkandarasi wa Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameagiza Wizara ya Maji kukaa pamoja na mkandarasi M. A. Kharafi & Sons ili kukubaliana namna bora ya kukamilisha kazi zilizobakia za mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unakamilika haraka.

Agizo hilo amelitoa leo Septemba 24, 2021 mara baada ya kukagua mradi huo unaotarajia kuhudumia zaidi ya wananchi 438,000 na kuitaka wizara ihakikishe vijiji vyote vinavyozunguka eneo la chanzo cha maji, eneo la Bwawa la Nyumba ya Mungu ilikowekwa miundombinu kuwa wanufaika wa kwanza wa mradi huo utakapokamilika.

Mhe. Majaliwa amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya majisafi na salama hivyo haitamvumilia mtu yeyote anayekwamisha utekelezaji wa mradi huo.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema pamoja na kazi nyingine mkandarasi huyo anatakiwa kuwezesha upatikanaji wa transfoma kwa ajili umeme ambazo zitawezesha usukumaji wa maji mpaka kwenye mtambo wa kutibu maji na hatimaye kusafirishwa kwenye matenki hadi kwa wananchi ajili ya matumizi.

"Nikuhakikishie kuwa tutaukamilisha mradi huu kwa wakati kwa kufanya kazi usiku na mchana na kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Same, Mwanga na Korogwe" amesema Aweso.

Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilion 262 na utakapokamilika utahudumia wananchi wapatao 438,000.