Habari

Imewekwa: Nov, 05 2019

Waziri Mbarawa akagua miradi ya maji Sikonge, Urambo na Kaliua

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amefanya ziara katika Halmashauri tatu za mkoa wa Tabora ambapo amekagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Urambo na Kaliua.

Waziri Mbarawa amefanya ziara hiyo ili kuona hali ya huduma ya maji na utekeleza wa miradi ya maji na changamoto zilizopo ili kuzipatia majibu.

Akiwa Sikonge Prof. Mbarawa ameona kupungua kwa kina cha maji katika bwawa na kujaa tope, pia uwepo wa magugu maji, uchakavu wa pampu za kusukuma maji na kuongezeka kwa uhitaji wa maji kutokana na ukuaji wa mji na idadi ya wananchi.

Waziri Mbarawa katika kutatua changamoto ametoa agizo pampu iliyopo Nzega ichukuliwe na kufungwa Sikonge ili huduma ya maji ipatikane kwa wananchi, na kusema Nzega watapata maji ya ziwa Viktoria katika kipindi kifupi kijacho.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Urambo kuwa watapata maji ya uhakika kutoka Ziwa Viktoria hivyo kuondokana na changamoto kubwa ya maji inayowakabili.

Aidha, akizungumza na wananchi wa Kaliua Waziri Mbarawa amewataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikijipanga kuwaletea maji kutoka Ziwa Viktoria mradi ambao utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika mji wa Kaliua pamoja na Urambo.

Wananchi wa Kaliua mjini kwa sasa wamepata mradi wa maji wa dharura ambapo utakapokamilika utaboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa kuzalisha lita 440,000 kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 42 ya mahitaji ya maji ya Mji wa Kaliua kwa sasa. Mradi huo wa dharura unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya Normar and Sons Co. Ltd ya Tabora kwa gharama ya Shilingi milioni 571,601,499.

Kitengo cha Mawasiliano