Habari
WaterAid Yakabidhi Mradi wa Maji Wenye Thamani ya Shilingi Milioni 465 Handeni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amepokea rasmi Mradi wa Usambazaji wa Huduma ya Maji ya Mtandao wa Mabomba wa Kwamaizi uliotekelezwa katika Kata ya Kideleko, Halmashauri ya Mji Handeni, Mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi huo, Mhandisi Mwajuma amesema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, usafi wa mazingira pamoja na usafi binafsi, kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa wananchi.
Mradi huo ulitekelezwa na WaterAid Tanzania kwa ufadhili wa OKF, kwa ushirikiano na Wizara ya Maji, Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM), pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni. Umegharimu jumla ya Shilingi 465,182,915.20 za Tanzania na unatarajiwa kunufaisha wananchi 6,037 katika maeneo ya Kideleko, Kampeni, Muungano, Ndekai na Bangu.
Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa chujio la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000, tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji lenye urefu wa mita 1,485, uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa mita 2,358, pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji vyenye mfumo wa malipo ya kabla.
Mhandisi Mwajuma amesisitiza HTM, RUWASA, viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa, kutunzwa na kusimamiwa ipasavyo ili huduma ya maji iendelee kuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Bi. Anna Mzinga, ameitaka RUWASA kwa kushirikiana na HTM pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza na kupanua huduma za mradi huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Bi. Mzinga amesisitiza kuwa usimamizi bora wa miundombinu ya mradi huo utahakikisha uwekezaji uliofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya na manufaa endelevu kwa jamii husika.

