Habari

Imewekwa: Aug, 31 2020

Watendaji Sekta ya Maji Watakiwa Kuimarisha Uadilifu na Ushirikiano

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewataka Watendaji wa Sekta ya Majikuimarisha uadilifu na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa wizara na taasisi zake katika kikao kazi cha kutathmini utendaji wa sekta ya maji kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu amefarijika na utendaji kazi wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kazi kubwa waliyoifanya ndani ya muda mfupi kwa kwa maeneo mengi ya vijijini kupata huduma ya maji tofauti na hali ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa wakala.

Mhandisi Sanga amebainisha kuwa RUWASA wamefanikiwa kukwamua miradi 97 kati ya miradi 177 iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu.

“Kwa kiasi kikubwa kero ya maji vijijini imepungua na wananchi wengi wanapata huduma ya majisafi na salama, ambapo wastani ya idadi ya watu wanaopata majisafi na salama vijijini imeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwezi Juni,2020”, Mhandisi Sanga alisema.

“Kwa upande wa mijini, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2020 baada ya kukamilika miradi 155 ya maji”, Mhandisi Sanga alisema.

Kwa ujumla Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) tangu mwaka 2007 hadi sasa jumla ya miradi 2,450 imetekelezwa mijini na vijijini. Kati ya hiyo, miradi 1,423 imetekelezwa kati ya mwaka 2015 na mwaka 2020 ambapo miradi 1,268 imetekelezwa vijijijini na miradi 155 imetekelezwa mijini.

Pamoja na hayo, Mhandisi Sanga amesisitiza ushirikiano wa watendaji wa taasisi zote za Wizara ya Maji ili kuweza kufanikisha malengo ya kuwafikishia Watanzania huduma ya maji ya uhakika.

Amezitaka Mamlaka za Maji nchini kutatua kero na kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao kwa kuzingatia kuwa bado yapo baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma ya maji.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Utumishi Dkt. Francis Michael amesisitiza kwa watumishi wa Wizara ya Maji kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu katika utumishi wa umma wakati wakutekeleza majukumu yao ya kila siku.