Habari
Wananchi wa Farkwa waanza kulipwa kupisha ujenzi wa bwawa
Serikali imetekeleza ahadi yake ya kulipa fidia wananchi wa Farkwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma ili kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la Farkwa.
Mkuu wa wilaya ya Chemba Bw. Simon Odunga akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la kulipa fidia amesema Serikali imetenga shilingi billioni 7.7 ili kuwalipa fidia wananchi wapatao 2,868 katika vijiji vya Mombose na Bubutole ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo.
Bw. Odunga amesema zoezi la kulipa fidia linatarajiwa kukamilika tarehe 31 Novemba, 2019 na kuwataka wananchi watakaolipwa kuhakikisha wanatekeleza notisi ya kuhama ndani ya miezi mitatu kuanzia tarehe 01 Novemba, 2019 hadi tarehe 31 Januari, 2020.
“Hakikisheni mnafuata sheria inayowataka kuhama ndani ya miezi mitatu, lakini serikali kwa kutumia busara inawaruhusu kwa kipindi hiki kutumia mvua zinazonyesha kulima mazao ya muda mfupi ili muweze kupata chakula ambacho mtakitumia huko mnakohamia,” Bw. Odunga alisema.
Mkuu wa Wilaya Bw. Odunga amewahakikishia wananchi hao kuwa kuanzia tarehe 01 Novemba, kikosi kazi cha maafisa ardhi kutoka katika ofisi yake kitaanza zoezi la kupima viwanja kwa ajili ya makazi katika eneo la Swakaleto na Manyata ambako wananchi hao watahamia.
Wakati huo huo, Bw. Michael A. Stio akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mombose na Bubutole amesema wanaishukuru sana serikali ya awamu ya tano kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwalipa fidia ili kupisha mradi mkubwa wa bwawa la maji ambalo litakuwa na manufaa makubwa kwa taifa, pia ameishukuru serikali kwa kuwaruhusu kulima mazao ya muda mfupi kwa kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha na kuahidi kuondoka katika maeneo watakayofidiwa.
Bwawa la Farkwa litakapokamilika litatumika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo maji kwa matumizi ya wakazi wa jiji la Dodoma.
Kitengo cha Mawasiliano

