Habari

Imewekwa: May, 20 2026

Ushirikiano Wahitajika Kulinda na Kuhifadhi Ziwa Victoria

News Images

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya Bonde la Ziwa Victoria kushirikiana kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za maji za ziwa hilo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho yanayoandaliwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria, yatakayofanyika Mei 21, Bw. Mtanda alisema kuwa Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu inayohudumia mamilioni ya wananchi katika nchi za Afrika Mashariki, hivyo linahitaji usimamizi na utunzaji wa pamoja.

Maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Nanenane, Nyamongoro, jijini Mwanza. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Bw. Mtanda alisisitiza kuwa maendeleo ya Jiji la Mwanza yanategemea kwa kiwango kikubwa uwepo wa Ziwa Victoria, kwani miradi mingi ya kimkakati ya maji, ikiwemo Mradi wa Maji wa Butimba, hutegemea ziwa hilo kama chanzo kikuu cha maji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Ambrose, alisema kuwa wizara imejipanga kuhakikisha wananchi wa Mwanza na maeneo mengine yanayozunguka ziwa hilo wananufaika ipasavyo na rasilimali ya maji kupitia juhudi za kuimarisha ulinzi, uhifadhi na maendeleo endelevu ya Ziwa Victoria.

Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawakilishi wa nchi wanachama wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha ushirikiano wa kikanda katika kulinda mazingira na rasilimali za Ziwa Victoria, ambalo ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya majisafi, uvuvi, usafiri na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.