Habari
Tutumie Teknolojia Kuleta Mageuzi Kwenye Sekta ya Maji

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kutumia teknolojia kuleta mageuzi zaidi katika Sekta ya Maji wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara ya Maji katika ofisi za Wizara hiyo Jijini Dodoma.
Amesema kuwa pamoja na mabadiliko na kazi kubwa inayofanyika katika sekta, kuna ulazima wa kutumia mfumo maalumu wa teknolojia utakaowezesha kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maji inayoendelea mijini na vijijini kwa ufanisi zaidi.
Amefafanua kuwa mifumo hiyo ni pamoja na mfumo maalum utakaotumika kufuatilia, kutoa taarifa za kila siku za utekelezaji wa miradi pamoja na usimamizi na uendeshaji wa miradi ili kuongeza ufanisi kiutendaji.
Aidha, Waziri Aweso ameishukuru menejimenti na watumishi wote wa Wizara ya Maji kwa ushirikiano mkubwa wanaompa na kusema kuwa mafanikio anayoyapata yanatokana na msaada mkubwa wanaompa kila siku.
Akisisitiza watendaji wote kuzingatia nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa Wizara anayoiongoza imelenga kuleta mabadiliko makubwa zaidi ya kisekta mwaka 2022.
“Nina uhakika na uwezo wa watumishi wote wa Wizara ya Maji, tufanye kazi kwa kujitoa na kujituma ili tumsaidie Rais Samia katika sekta yetu ya maji”, amesema Aweso.
Pia, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka watumishi wote kuongeza ushirikiano zaidi ili kwa pamoja waweze kutimiza malengo ya Serikali ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama vijijini na mijini.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewapongeza viongozi wa wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia sera na kusema Wizara itahakikisha changamoto zote za upatiukanaji wa huduma ya maji kwa wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.