Habari

Imewekwa: Mar, 17 2020

Tahadhari Kuhusu Mabwawa

News Images

Wizara ya Maji inapenda kuwataarifu wananchi wote wakiwemo wamiliki wa mabwawa ya maji na mabwawa ya tope sumu kuzingatia matangazo ya utabiri wa hali ya hewa yanayotolewa kuhusu mvua za masika za mwaka huu kuwa juu ya wastani katika maeneo mengi nchini.

Mvua hizi zinaweza kusababisha mabwawa kujaa maji zaidi ya uwezo wake hivyo kutishia usalama wa wananchi, mali zao na mazingira kwa ujumla. Mabwawa yanaweza kupasuka kwa sababu ya kujaa au kutiririsha maji katika mikondo isiyo rasimi (overflow) na miongoni mwa madhara yake ni kuleta mafuriko katika vijiji, barabara, madaraja na kuharibu miundombinu mingine. Hivyo, Wizara inawataka wamiliki wote wa mabwawa ya maji kutekeleza yafuatayo;

  • 1. Kusafisha utoro wa maji, kuimarisha tuta la bwawa kwa kuondoa miti yenye mizizi na vichuguu juu ya tuta, kuziba matoleo yote yanayotumika kutolea maji wakati wa kiangazi (Dry spell draw off points) na kutunza uoto wa asili ili kudhibiti uingiaji wa mchanga (sediments) kwenye bwawa ikiwemo kupanda mimea/miti rafiki ya kupunguza kasi ya kuingiza michanga kwenye bwawa.
  • 2. Wamiliki wote wa mabwawa ya tope sumu kuhakikisha wanadhibiti maji ili yasisambae katika mazingira. Hii ni pamoja na kuboresha miundombinu iliyopo ili kutoruhusu maji yenye sumu kutiririka na kuchafua mazingira. Aidha, Wizara inawataka wananchi wote wanaoshi chini ya utoro wa maji wa mabwawa (downstream) na wale wanaoishi kuzunguka migodi kuchukua tahadhari kutokana na mabwawa kujaa maji zaidi ya uwezo wake.
  • 3. Wamiliki wote wa mabwawa wanatakiwa kuwasilisha mipango ya usalama wa mabwawa na mafuriko kwa Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji ili kukabili dharura itakayotokea kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kama Sheria ya Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009 sehemu ya X na Kanuni zake za Usalama wa Mabwawa GN. 237 za mwaka 2013 kifungu cha 16 inavyoelekeza.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini