Habari
Serikali Kutumia Chuo cha Maji Kutatua Changamoto za Miradi ya Maji

Dar es Salaam; 03 Januari, 2020
TAARIFA KWA UMMA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameitaka Wizara ya Maji kuandaa mkakati maalum wa kukifanya Chuo cha Maji kuwa sehemu ya suluhisho ya changamoto zinazoikabili Sekta ya Maji kwa kutumia wataalam wanaozalishwa na chuo hicho kutimiza lengo la sekta la kuwapatia wananchi huduma ya majisafi na salama.
Naibu Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Menejimenti ya Chuo cha Maji akisema wizara imedhamiria kuwatumia wataalam wanaotoka kwenye chuo hicho kutatua changamoto mbalimbali katika utekelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji kama ilivyokuwa lengo la kuanzishwa kwake.
Mhe. Aweso amesema Chuo cha Maji ni uti wa mgongo wa Wizara ya Maji na kilianzishwa kwa dhumuni la kuzalisha wataalam watakaotumika kwenye Sekta ya Maji, hivyo kuna haja ya kuweka utaratibu maalum ili kukisaidia kuwa na mfumo mzuri wa kupata wataalam bora zaidi watakaokuwa msaada mkubwa kwa Serikali.
“Miradi ya maji 153 iliyogharimu Shilingi bilioni 68 katika maeneo mbalimbali ina changamoto, tutumie wataalam kutoka Chuo cha Maji ambapo Serikali inatoa ruzuku kiweze kujiendesha na kuzalisha wataalam watakaotusaidia kurekebisha kasoro zote’’, amesema Naibu Waziri Aweso.
“Tutumie wataalam hawa kwenda kutatua changamoto za miradi yetu, lakini pia tuwajengee uwezo wa kuweza kusimamia na kuendesha miradi ya maji ili tuachane na wataalam ambao wengi wao gharama zao ni kubwa na kwa sehemu kubwa wamezorotesha sana utekelezaji miradi ya maji’’, amesema Mhe. Aweso.
Aidha, Naibu Waziri Aweso ameutaka uongozi wa Chuo cha Maji kuimarisha idara zake kwa lengo la kuongeza ufanisi utakaowajengea uwezo zaidi wanafunzi wake watakaoweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Maji.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maji, Dkt. Adam Karia amesema wamejipanga kuimarisha uwezo wa chuo hususan kwa upande wa mitaala na utaalam kwa wafanyakazi ili kuhakikisha kinakidhi mahitaji ya kisekta.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini