Habari
Zaidi ya Wananchi 6,961 Waondokana na Kero ya Maji Mkoani Kagera
Zaidi ya wananchi 6,961 wa Vijiji vya Nsisha, Kagoma na Kikuku wilayani Muleba, mkoani Kagera, wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama baada ya Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutekeleza mradi mkubwa wa maji.
Mradi huo umeleta faraja kubwa kwa wakazi wa Kata ya Kikuku, ambapo Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 ziliweka jiwe la msingi, ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma ya maji vijijini.
Ashura Juma, mkazi wa Kagoma, amesema changamoto ya maji imekuwa kikwazo kwa miaka mingi, hususan nyakati za kiangazi ambapo watoto walilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji, hali iliyosababisha mateso na madhila ya kijinsia pamoja na adhabu kutoka kwa wazazi. “Kwa sasa tuna matumaini makubwa, watoto wetu hawatapata mateso haya tena,” Ashura amesema kwa furaha.
Naye Zida Milanga, mkazi wa Kikuku, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji katika maeneo ya pembezoni, akisema hatua hiyo imeondoa adha kubwa kwa wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Muleba, Mhandisi Paschale Kibangule, amesema mradi huo umegharimu shilingi milioni 650 na umefikia asilimia 89 ya utekelezaji. Tayari wananchi wameanza kuunganishiwa huduma za maji nyumbani, ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 25, 2025.
Mhandisi Kibangule amebainisha kuwa kazi zilizotekelezwa mpaka sasa ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 150,000, ujenzi wa chanzo cha maji (intake), mtandao wa mabomba wa kilomita 14.7, ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji pamoja na ujenzi wa ofisi za Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs).
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanalinda na kutunza vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

