Habari

Imewekwa: Oct, 31 2019

Mradi wa Maji wa Kisarawe kuanza Kutoa Maji Mwezi Ujao

News Images

Dar es Salaam: 31 Oktoba, 2019

TAARIFA KWA UMMA

Mradi wa Maji wa Kisarawe kuanza Kutoa Maji Mwezi Ujao

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametembelea na kukagua utekelezaji wa kazi ndogo zilizobaki katika ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kisarawe katika Kata ya Kibamba, wilayani Ubungo.

Ziara imelenga kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa jana kwa mkandarasi kukamilisha utaratibu wa malipo na kazi ya kuvuta umeme ifanyike haraka ili mradi uanze kufanya kazi mwezi ujao.

Malipo ya Shilingi milioni nane kwa TANESCO yameshafanyika na kazi ya kufunga umeme huo itaanza mara moja tayari kwa kufanya majaribio ya kusukuma maji (pump test) wiki ijayo.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Aweso ameambatana na Wakuu wa Wilaya za Ubungo, Kisare Makori na Kisarawe, Jokate Mwegelo akiwasisitiza umoja na ushirikiano katika kufanikisha zoezi la utekelezaji wa mradi huo kwa maslahi mapana ya wananchi wa Kisarawe.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori ametoa rai kwa viongozi na watendaji wa wilaya za Ubungo na Kisarawe kujitoa na kusimamia miradi ya maendeleo inayotumia fedha nyingi, hatua itakayosaidia juhudi za Serikali kuzaa matunda.

Kitengo cha Mawasiliano.