Habari

Imewekwa: Jun, 17 2022

Mfumo wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji Kuchochea Maendeleo ya Taifa

News Images

Mwenyekiti wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji (National Multi-Sectoral Water Resources Management and Development Forum), Mhandisi Mbogo Futakamba amesema Serikali imeweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa rasilimali za maji nchini kuhakikisha zinasimamiwa na kuendelezwa ipasavyo kwa manufaa ya taifa kwa miaka mingi ijayo.

Mhandisi Futakamba ametoka kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Kamati ya Uendeshaji ya Jukwaa hilo (Forum Steering Committee) na cha Vikundi Kazi (Working Groups) katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

''Kupitia mfumo huu usimamizi wa rasilimali za maji unafanyika kuanzia ngazi ya chini ya watumia maji kwa kuunda Jumuiya za Watumia Maji ikifuatiwa na Kamati za Maji za Mabonde Madogo, Bodi za Maji za Mabonde mpaka ngazi ya juu ya Bodi ya Maji ya. Taifa", Mhnadisi Futakamba amefafanua.

"Utaratibu huu unaongozwa na Sera ya Maji ya Taifa ya mwaka 2002 na Seria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009, pamoja na sheria za sekta nyingine mtambuka za mazingira, misitu na ardhi", Mhandisi Futakamba amesema.

Vilevile, Mhandisi Futakamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa (National Water Board) amesema kuwa lengo kuu la kikao cha Kamati ya Uendeshaji ni kuupitisha Mpango Mkakati wa Jukwaa kwa mwaka 2022/2023 ili kuwa na mwongozo na mfumo mzuri wa uendeshaji wa jukwaa.

Malengo mengine ya kikao hicho ni kupitia hadidu za rejea za vikundi kazi, kuwezesha utekelezaji mzuri wa maamuzi ya jukwaa na namna ya kupima matokeo, pamoja na kuandaa mikakati ya uendelevu wa jukwaa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe takribani 90 kutoka sekta, taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali.