Habari

Imewekwa: Sep, 24 2020

Matokeo ya Kazi Yetu ni Wananchi Kupata Maji-Mhandisi Kemikimba

News Images

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka watendaji katika sekta ya maji nchini kuhakikisha matokeo ya kazi zao ni wananchi kupata huduma ya maji ya uhakika.

Mhandisi Kemikimba amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akishiriki mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa sekta ya maji watakaofanya kazi ya kuzijengea uwezo bodi za wakurugenzi wa mamlaka za maji hasa katika menejimenti ya mamlaka hizo.

“Mhakikishe mafunzo mtakayoyatoa kwa bodi za wakurugenzi wa mamlaka za maji nchini yanasaidia kufikia malengo ya sekta yetu ya maji na ya kitaifa kwa kuwapatia wananchi huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza” Mhandisi Kemikimba amesema.

Aidha, amewashauri washiriki wa mafunzo kuzingatia suala la Ufuatiliaji na Tathmini katika ufundishaji wao ili hatimaye serikali iweze kujua huduma ya maji kwa wananchi inapatikana kwa kiwango gani katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mhandisi Kemikimba amesema kuongea lugha moja katika huduma ya maji ni jambo la msingi, hivyo ni muhimu kujua wananchi wanapokeaje huduma hiyo na mrejesho wao ufanyiwe kazi kwa haraka.

Mamlaka za maji ni matokeo ya mabadiliko yaliyofanywa na serikali miaka ya 90 ambapo zilikasimiwa madaraka ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi.

Kitengo cha Mawasiliano