Habari
“Marufuku Ujenzi wa Miradi bila Kuwa na Chanzo cha Maji cha Uhakika”

Morogoro; 17 Disemba, 2019
TAARIFA KWA UMMA
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa onyo kali kwa wahandisi wa maji nchini kutoanza kazi yoyote ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji bila kupata chanzo cha maji cha uhakika.
Onyo hilo limekuja baada ya kukagua Mradi wa Maji wa Gwata uliopo katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro na kukuta changamoto ya chanzo cha maji cha Chalinze, mkoani Pwani kuwa kuwa kikwazo cha mradi huo kushindwa kutoa maji.
Taarifa ya mradi huo iliyosomwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Grace Lyimo imeonyesha kuwa tatizo la chanzo tarajiwa kilichopo Chalinze, mkoani Pwani kilichokuwa kitumike kushindwa kufikisha maji katika Kata ya Gwata licha ya kazi za ujenzi wa matenki mawili, vituo vya kuchotea maji na ulazaji wa mabomba ikiwa inakaribia kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 261.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Gwata, Mhe. Aweso amesikitishwa na kitendo hicho ambacho kimesababishwa na kukosewa kwa usanifu na kuitaka RUWASA kufika kwenye mradi huo kuuangalia, akisema kitaalam kosa hilo ni kubwa na hakutegemea kosa kama hilo lifanywe na watu wenye uwezo na kazi za uhandisi.
Akaielekeza TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na kuihoji Kampuni ya Don Consult iliyofanya usanifu wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini, Mhandisi Mkama Bwire amesema kiufundi mradi huo umekosewa usanifu, hivyo watabaki Gwata pamoja na timu ya wataalam RUWASA kuupitia na kufanya usanifu upya ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa pamoja na kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu kutafuta chanzo mbadala kilicho karibu zaidi katika Mkoa wa Morogoro baadala ya Pwani.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimuomba Naibu Waziri wa Maji kuupatia ufumbuzi haraka mradi huo uweze kukamilika kwa kuwa umechukua muda mrefu tangu ujenzi wake uanze, pamoja na wananchi kuwa na matumaini makubwa na mradi huo kumaliza tatizo la maji linalowakabili.
Mradi wa Maji wa Gwata ulisanifiwa mwaka 2015 kwa lengo la kuhudumia wakazi 2,509 na ujenzi wake ulianza Julai, 2015 chini ya Mkandarasi, MS Kumba Quality Co. Ltd kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 440.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini