Habari
Katibu Mkuu aiwakilisha sekta katika mkutano wa Cop29 nchini Azerbaijan
Uimarishaji wa usimamizi wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika mabonde ya maji
Mhandisi Mwajuma Waziri - Katibu Mkuu Wizara ya Maji, jana tarehe 13 Novemba, 2024 akiendelea kushiriki mkutano wa CoP29 nchini Azerbaijan alishiriki mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika kupungua kwa mabonde ya maji (Adverse Impacts of Climate Change on the Decline of Water Basins). Mkutano ulizinduliwa na Mhe. Mukhtar Babayev Rais wa COP29 ambaye ni Waziri wa Ikolojia na Maliasili nchini Azerbaijani pamoja na Mhe. Retno L.P Marsudi Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji (UN Water Envoy).
Mkutano uliangazia masuala ya kupungua kwa rasilimali maji katika mabonde duniani huku majadiliano yakijikita katika masuala mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu, sera, kukuza ushirikiano wa kimataifa hasa baina ya mataifa yenye kutumia maji shirikishi, njia bora na mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Kupitia mkutano huo uliohusisha mjadala wa jopo la mawaziri wa masuala ya Mazingira, Maji na Mabadiliko ya Tabianchi wa nchi za Bolivia, Chad, Uganda, United Arab Emirates, Iran, Azerbaijan, Kazakhstan na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa kama vile IPPC, IFAD CICA na UNECE, Tanzania inaimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji yakiwemo maziwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.