Habari

Imewekwa: Nov, 11 2020

Huduma ya Maji ni Nyenzo ya Msingi katika Kuondosha Umasikini

News Images

Upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubora wa maisha, kupunguza makali ya athari zinazotokana na umaskini na kuongeza kipato cha wananchi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema hayo wakati wa kikao kazi chaBodi za Wakurugenzi kinachofanyika mjini Njombe na kuhusisha bodi za Wakurugenzi kutoka mamlaka 15 zinazotoa huduma ya majisafi kwa wananchi.

Mhandisi Sanga, katika kikao hicho, amesema tafiti za afya zinaonesha kuwa upatikanaji wa majisafi na salama hupunguza zaidi ya asilimia hamsini ya magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na maji yasiyo salama, na kusisitiza kuwa kwa kutambua umuhimu huo wa maji kwa afya na maendeleo ya wananchi, lengo la Serikali ni kuwafikishia wananchi wote huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100.

Kuhusu Bodi za Wakurugenzi, ameongeza kuwa moja ya majukumu ya bodi hizo ni kushughulikia malalamiko ya Watumishi na wateja wa mamlaka za maji kwa wakati na kuhakikisha mamlaka zinakuwa na mipango ya kupanua utoaji wa huduma katika maeneo yake na kuwakumbusha wajumbe wa bodi kuwa wamepewa dhamana kubwa na Waziri wa Maji aliyewateuwa ili kufanikisha kazi ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wote.

Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira zinazoshiriki kikao kazi ni Mamlaka ya Mbeya, Iringa, Tabora, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Mtwara, Makambako, Wanging’ombe, Mafinga, Tukuyu, MANAWASA, Makonde, Chunya na Kyela Kasumulu.

Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira ni Taasisi za Serikali zinazojitegemea ambazo zilianzishwa mwaka 1997 kupitia akaunti maalum chini ya Sheria ya Mwaka 1961 (Cap Ordiance 281 Misceleneous Ammendment ACT). Baadae ilitungwa Sheria Na. 12 ya Majina Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009 ambayo ilzitambua mamlaka. Hivi sasa mamlaka ipo Sheria Namba5 ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 ambayo pamoja na mengine imezitambua mamlaka na kuboresha masuala mbalimbali kuziongezea ufanisi katika kutoa huduma ya majisafi kwa Watanzania.

Kitengo cha Mawasiliano