Habari
Hizi hapa fursa za Tanzania katika sekta ya maji - Mhandisi Mwajuma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amebainisha fursa zilizopo nchini Tanzania na umuhimu wa kuwa na miradi ya maji na mabadiliko ya maji ambayo ni jumuishi.
Amesema kuwa fursa hizo ni hatua itakayosaidia katika kutoa huduma kwa sekta mtambuka na matokeo makubwa kwa jamii.
Mhandisi Mwajuma ameweka hayo bayana aliposhiriki katika mjadala uliohusu Usalama wa Maji na Uhimilivu wa Mabadilko ya Tabianchi Barani Afrika (Water Security for Climate Resilience in Africa: Transformative Water Systems for Climate Adaptation) ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) kwa kushirikiana na chombo chake cha Africa Water Facility (AWF)
Mhandisi Mwajuma amebainisha uhitaji wa fedha, uwezo wa kitaasisi wa kuandaa miradi na umuhimu wa mifumo jumuishi inayounganisha sekta mtambuka katika usimamizi, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu ya maji na mabadiliko ya tabia nchi kama maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele katika uwekezaji.
Amewahakikishia wajumbe kuwa Tanzania ni eneo salama na kwamba Wizara ya Maji na serikali kwa ujumla iko tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa katika makubaliano mbalimbali yanafikiwa.
Mjadala ulifanyika katika Banda la Mabenki ya Maendeo (Multilateral Development Banks - MDBs), pembezoni mwa Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28) unaofanyika Jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mjadala ulilenga dhana ya usalama wa maji na uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.