Habari
Serikali Yaendelea Kuimarisha Huduma ya Maji Mwanza
Hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu huduma ya maji jijini Mwanza imeonesha matokeo mazuri kwa huduma hiyo kuendelea kuimarika.
Waziri Aweso ameyasema hayo wakati akiendelea na ziara ya siku nne ya kukagua utekelezaji wa hatua mbalimbali za kutatua changamoto ya huduma ya maji katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana.
Akiwa katika Kata ya Buswelu, wilayani Ilemela, Waziri Aweso ameshuhudia tenki la maji la ujazo wa lita milioni tatu likiwa limejaa na kuanza kusambaza maji kwa wananchi wa maeneo jirani.
“Hii ni siku yangu ya nne nikiwa Mwanza, na naridhishwa na hatua zinazochukuliwa kwa sababu huduma inaendelea kuimarika,” Aweso amesema.
Amebainisha kuwa baadhi ya maeneo ya Ilemela na Nyamagana tayari huduma ya maji imerejea na wananchi wameanza kupata maji.
Aweso amesisitiza watendaji wote wa Sekta ya Maji katika ngazi zote nchini kufanya kazi inayozingatia matokeo kwa mwananchi.
“Lazima tuwe na utaratibu mzuri wa utoaji huduma. Kama kuna mgao, ratiba za maji ziwe wazi na za kutabirika. Na kama kuna changamoto, taarifa ziwafikie wananchi kwa wakati,” Aweso amesisitiza.
Aidha, Waziri Aweso amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kuendelea kutembelea maeneo mbalimbali jijini Mwanza ili kusimamia kwa karibu utatuzi wa changamoto na kuhakikisha huduma imerejea kwa wananchi.

