Habari

Imewekwa: Oct, 26 2023

​Bilioni 42 zinatekeleza miradi ya maji Makambako - Aweso

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetengakiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Mlowa, Kijiji cha Idofi mkoani Njombe.

Amesema hayo katika kijiji cha Idofi akiwa katika msafara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango anayefanya ziara mkoani Njombe.

Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi wa maji na kwamba fedha hizo shilingi bilioni 3.2 zitakamilisha mradi hu na kumuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Makambako kuanza mara moja utekelezaji wa mradi huo.

Sanjari na hilo, Waziri Aweso amemuhakikishiaMakamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango kuwa fedha shilingi bilioni 42 zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maji katika mji wa Makambako zitakamilisha miradi yote kwa wakati ili kuwaondolea wananchi uhaba wa huduma ya majisafi.

Pamoja na hayo, Waziri Aweso ameridhia ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, Mhe. Deo Sanga ambaye ameomba Wizara ya Maji kujenga Tenki kubwa la maji katika kata ya Mlowa, kijiji cha Idofi-Makambako ambapo kazi hiyo itatekelezwa kupitia mradi wa maji wa Mlowa wenye thamani ya shilingi bilioni 3.2.

Mhe. Sanga amempongeza Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kwakazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Maji katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Miji 28 ambapo Mkoa wa Njombe ni sehemu ya mradi huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdori Mpango yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe ambayo ameanza leo.

Kitengo cha Mawasiliano