Habari
Aweso atoa siku 30 mradi wa maji Seluka kukamilika

Tazama Video ya tukio hili kwa kubofya HAPA
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemuagiza Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mpwapwa Mhandisi Cyprian Warioba kuhakikisha ndani ya siku 30 changamoto ya huduma ya maji katika kijiji cha Seluka Wilayani Mpwapwa inapatiwa ufumbuzi.
Agizo hilo amelitoa akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji wilayani Mpwapwa ambapo aliongozana na viongozi wengine wa serikali akiwemo mbunge wa jimbo la Kibakwe Mhe George Simbachawene.
“Meneja Tanesco amezungumza hapa kuwa ndani ya siku 30 umeme utakuwa umefika hapa, kwa hiyo huna kisingizio. Ndani ya siku 30 wananchi wa Seluka wawe wamepata huduma ya maji. Amesema Mhe. Aweso
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Mpwapwa Mhandisi Cyprian Warioba alisema mradi huo ulisimama kufanya kazi kutokana na hitilafu ya umeme iliyopelekea kuungua kwa genereta iliyokuwa ikiendesha mitambo ya mradi huo. Hii ilipelekea kijiji kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibakwe kilipo kijiji hicho Mhe. George Simbachawene ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali kwani ina nia ya dhati ya kuhakikisha changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi.
Mradi wa maji kijiji cha Seluka ni miongoni mwa miradi tisa ya maji iliyotekelezwa ndani ya Wilaya ya Mpwapwa kupitia Mpango wa Program ya Maendeleo ya Maji Awamu ya Pili (WSDP II).