Habari
Huduma ya Majisafi Yazidii Kuimarika Mwanza.
Huduma ya majisafi imezidi kuimarika katika jiji la Mwanza baada ya Serikali kuchukua hatua muhimu kutatua kero ya maji kwa wananchi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameendelea kusimamia zoezi la kitaalam kurejesha huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Maeneo ya Buswelu, Nyegezi na Igoma wakazi wake wameeleza kufurahishwa kwa kurejea huduma ya maji baada ya kuikosa kwa siku kadhaa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara ya Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma wananchi walikiri kuwa huduma hiyo imerejea na maisha kurudi katika hali ya kawaida.
Mhandisi Mwajuma, akiwa ameambatana na viongozi wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wataalamu wa Sekta ya Maji, amekagua maeneo mbalimbali kujionea hali halisi.
“Nimetembelea Kata za Buswelu, Nyegezi na Igoma na hali ya upatikanaji wa huduma inaendelea kuimarika baada ya wataalamu wetu kuchukua hatua stahiki,” Mhandisi Mwajuma amesema.
Amesisitiza kuwa uwazi na uwajibikaji wa wataalamu wa Sekta ya Maji ndio suluhu ya kudumu ya changamoto na utasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi.
“Tuzingatie Mkataba wa Huduma kwa Mteja, kazi yetu ni kutatua changamoto zote kwa haraka na kuzishughulikia hoja za wananchi kwa wakati, kabla hazijawa kubwa,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mwajuma amesema kazi ya maunganisho ya wateja wapya inaendelea kwa kasi mara baada ya vifaa vya kutosha kuwasili Mwanza.
Amewataka wananchi wanaohitaji huduma ya maji kuwasilisha maombi yao kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ili waweze kuunganishiwa.

