Habari

Imewekwa: Jun, 19 2026

Wadau wa Maendeleo Kushirikishwa Uimarishaji Huduma ya Maji Mwanza

News Images

Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi jijini Mwanza.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amefanya kikao na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Mhe. Christine Grau, kujadili hatua za utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maji na Usafi wa Ziwa Victoria (LVWATSAN).

Amesema Serikali inathamini mchango mkubwa wa EU katika sekta ya maji, na Jijini Mwanza ambako mahitaji yanaongezeka kutokana idadi ya watu na ukuaji wa mji.

Ametoa shukrani kwa EU kwa ushirikiano utakaowezesha MWAUWASA kumaliza changamoto ya mgao wa maji na kupanua wigo wa huduma.

Balozi wa EU nchini Mhe. Grau amesema umoja huo umeridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika kuboresha utoaji huduma na kuimarisha uwazi, na wapo tayari kuunga mkono juhudi hizo.

EU na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), kwa kushirikiana na Wizara ya Maji wanatarajia kusaini Hati ya Makubaliano yenye thamani ya takribani Euro milioni 12.5.

Makubaliano hayo yatawezesha upatikanaji wa fedha kuanza utekelezaji wa programu ya LVWATSAN Awamu ya Pili, ikijumuisha upanuzi wa mtandao wa mabomba, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa mfumo wa majitaka Jijini Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ameeleza kuwa usafi wa mazingira ni eneo muhimu la uwekezaji, hususan kwa wakazi wanaoishi maeneo ya miinuko na pembezoni mwa jiji.

EU ni mdau wa maendeleo anayeshirikiana na Wizara ya Maji katika utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira.