Habari

Imewekwa: Jun, 20 2026

Tanzania na Ujerumani Zaendeleza Ushirikiano Katika Sekta ya Maji

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amefanya mazungumzo na Kaimu Mkuu wa Idara ya Miradi ya Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani nchini. Bi. Marlene Landes, jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yamejikita katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani katika Sekta ya Maji.

Mhandisi Mwajuma amesisitiza ushirikiano ujikite zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuongeza tija.

Ametaja umuhimu wa kujenga uwezo wa wataalamu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia, kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya SCADA katika uendeshaji na ufuatiliaji wa miundombinu.

Ameongeza kuwa kuna haja ya kuendeleza matumizi ya Hati Fungani za Kijani kama chanzo mbadala cha fedha za uwekezaji, pamoja na kuhimiza matumizi ya vifaa vinavyotumia nishati ya jua vyenye ufanisi mkubwa.

Mhandisi Mwajuma amebainisha kuwa Sekta ya Maji bado inahitaji vyanzo mbadala vya fedha na ushirikiano wa kiufundi ili kuharakisha utekelezaji na ukamilishaji wa miradi nchini.

Aeishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia KfW na GIZ kwa mchango wake katika kufanikisha malengo ya sekta na kuboresha huduma za maji.

Bi. Landes alithibitisha dhamira ya Serikali ya Ujerumani kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika Sekta ya Maji, akibainisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.