Habari
Ushirikiano wahitajika kutunza ziwa Victoria
Ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii unahitajika katika kutunza ziwa Victoria.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amewataka wananchi wa eneo la kamisheni ya Bonde la ziwa Victoria kushirikiana katika utunzaji wa rasilimali maji ya ziwa hilo.
Amesema hayo akifungua maonesho kuelekea siku ya Ziwa Victoria ambayo itafanyika Mei 21.
Maonesho yanafanyika katika eneo la Nyamongoro viwanja vya Nanenane jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi katika siku ya ziwa Victoria anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mkuu wa Mkoa Bw. Mtanda amesema ziwa Victoria lina umuhimu mkubwa kwa wananchi wote za nchi za Afrika Mashariki hivyo ushirikiano wa dhati unahitajika kuwezesha rasilimali hiyo kuendelezwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesisitiza kuwa mstakabali wa jiji la Mwanza ni uwepo wa ziwa Victoria kwa sababu miradi mikubwa ya kimkakati ya maji ukiwemo mradi wa maji wa Butimba chanzo chake ni ziwa Victoria.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Ambrose amesema Wizara ya Maji imejipanga kuhakikisha wananchi wa Mwanza wananufaika na rasilimali ya maji kwa kuhakikisha ulinzi na uendelezaji wa ziwa Victoria unapewa kipaumbele.
Siku ya Ziwa Victoria inatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa nje na ndani ya nchi wakiwemo nchi zinazounda Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, nchi za Tanzania, Kenya Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

