Habari
Wadau Waalikwa Kuwekeza katika Uhifadhi wa Ziwa Victoria
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Rose Ambrose, ametoa wito kwa washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kuwekeza katika uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji za Ziwa Victoria. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa Bonde la Ziwa Victoria iliyofanyika jijini Mwanza katika maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria, Bi. Ambrose alisema kuwa juhudi za kulinda na kuendeleza ziwa hilo zinahitaji rasilimali za kutosha, uratibu madhubuti na ushirikiano wa karibu katika ngazi zote. Alieleza kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa zinazohusiana na maji, zikiwemo upungufu wa maji, ukame, mafuriko, uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alibainisha kuwa changamoto hizo zimevuka mipaka ya kiutawala na kitaifa, hivyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. “Maji yanatukutanisha na kutulazimisha kushirikiana kwa manufaa ya wote,” alisema. Bi. Ambrose aliwahimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, jumuiya ya kimataifa, washirika wa maendeleo, wataalamu, watafiti, asasi za kiraia na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi na kulinda Ziwa Victoria. Alisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuwa balozi wa uhifadhi wa ziwa hilo kwa kushiriki katika shughuli za uhifadhi na kupinga vitendo vinavyohatarisha mazingira na rasilimali zake. “Endapo kila mmoja wetu atachukua jukumu la kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria, tutafanikiwa kuhakikisha rasilimali hii muhimu inaendelea kunufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” alisema. Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi chini ya kaulimbiu isemayo: “Maji Yetu, Mustakabali Wetu: Tuungane kwa Usimamizi Endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria.”

