Habari

Imewekwa: May, 19 2026

Serikali Kumaliza Adha ya Maji Chemba Kupitia Mradi wa Bilioni 11

News Images

Serikali imeahidi kumaliza kabisa adha ya uhaba wa maji kwa wakazi wa Mji wa Chemba kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa na Wizara ya Maji.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba alisema Serikali itahakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.

“Chemba imekuwa ikikumbwa na changamoto ya ukame na uhaba wa maji. Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika,” alisema Dkt. Nchemba.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Usambazaji Maji wa Wizara ya Maji, Mhandisi Charles Mafie, mradi huo una thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 11 na utekelezaji wake umefikia asilimia 76.

Alieleza kuwa mradi unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 18,000 wa Mji wa Chemba na vijiji vya Chemba, Chambalo, Kambi ya Nyasa, Gwandi, Paranga na Makamaka.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha jumla ya lita 207,000 kwa saa, ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji, kituo cha kusukuma maji, pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji yenye urefu wa kilomita 60.

Baada ya kukamilika, upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo hilo unatarajiwa kupanda kutoka asilimia 37 ya sasa hadi asilimia 100. Uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka wastani wa lita 170,000 kwa siku hadi zaidi ya lita milioni 3 kwa siku, hatua itakayobadilisha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.