Habari

Imewekwa: May, 19 2026

Ushirikiano Wahitajika Kulinda na Kuendeleza Ziwa Victoria – RC Mtanda

News Images

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi rasilimali za Ziwa Victoria kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhe. Mtanda alitoa wito huo wakati akifungua rasmi maonesho ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yanayotarajiwa kufanyika Mei 21, 2026.

Maonesho hayo yanafanyika katika Viwanja vya Nyamongoro Nanenane, jijini Mwanza. Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu inayowahudumia wananchi wa nchi zote za Afrika Mashariki, hivyo linahitaji juhudi za pamoja kulilinda. Aliongeza kuwa mustakabali wa Jiji la Mwanza unategemea moja kwa moja uwepo wa ziwa hilo, akitolea mfano Mradi mkubwa wa Maji wa Butimba ambao chanzo chake kikuu ni Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Ambrose, alisema Wizara imejipanga kuhakikisha ulinzi na uendelezaji wa Ziwa Victoria unapewa kipaumbele ili wananchi wa Mwanza na maeneo mengine wanufaike na rasilimali hiyo kwa uendelevu.

Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria: Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.