Habari
Mkandarasi Atakiwa Kuharakisha Ukamilishaji wa Mradi wa Maji Miji 28 Mafinga
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Rose Ambrose, ameitaka Kampuni ya Jandu Plumbers Ltd kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 Mafinga ili wakazi wa Mafinga na maeneo jirani ya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, waanze kunufaika na huduma ya majisafi na salama.
Bi. Rose amesema kuwa hajaridhishwa na maendeleo ya mradi ambayo imefikia aslimia 20.5 ya utekelezaji wake na kusisitiza mkandarasi ana kazi kubwa ya kufanya. Akimtaka kuweka nguvu kubwa kukamilisha kazi iliyobaki.
Ameeleza kuwa mkandarasi huyo hana sababu ya msingi ya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo, kwani malipo yote anayodai yameshalipwa na hati zote za madai alizowasilisha awali zililipwa kwa wakati.
“Serikali tayari imekulipa takriban shilingi bilioni 14, na hati mbili za mwisho za madai zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.2. Nataka uendelee na kazi. Huna sababu yoyote ya msingi inayosababisha mradi kusuasua,” Bi. Rose amesisitiza.
Amebainisha kuwa maendeleo ya kazi yaliyofikia asilimia 20.5 hadi sasa iko chini ya kiwango na hayaendani na asilimia 29 ya malipo ambayo mkandarasi ameshalipwa. Amesisitiza kuwa malipo ya fedha yanatakiwa yaendane na utekelezaji wa mradi huo.
“Fedha nyingi za Serikali zimeshatolewa na wewe mwenyewe umethibitisha hilo. Hatutakubali kuona mradi ukiendelea kuchelewa. Ni lazima tuone mpango kazi wako na ujenzi wa bwawa ambalo ndilo chanzo kikuu cha mradi huu uanze mara moja,” Naibu Katibu Mkuu ameongeza.
Amesema kuwa ujenzi wa tenki la maji na miundombinu mingine hautakuwa na maana iwapo itakamilika pasipo maji kutoka.
Naibu Katibu Mkuu amefanya ziara ya kikazi mkoani Iringa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mradi huo unaogharimu takriban shilingi bilioni 48. Mradi huo unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama katika Mji wa Mafinga kutoka asilimia 67 kwa sasa hadi asilimia 89.
Mradi huo utanufaisha zaidi ya wakazi 109,720 wa kata saba za Boma, Changarawe, Rungemba, Wambi, Upendo, Kinyanambo na Sao Hill, kati ya kata tisa zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga.

