Habari

Imewekwa: May, 19 2026

Miti 2,000 Yaoteshwa Chanzo cha Maji Butimba Siku ya Ziwa Victoria

News Images

Wananchi katika mkoa wa Mwanza wameshiriki kampeni ya kutunza vyanzo vya maji katika ziwa Victoria kwa kuanza kuotesha miti elfu mbili katika chanzo cha maji cha Butimba.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameongoza zoezi hilo ambapo miti rafiki wa maji imeoteshwa kuashiria uzinduzi wa kampeni ya kuotesha miti kuelekea siku ya ziwa Victoria ambayo inaadhimishwa kwa mara ya kwanza Jijini Mwanza.

Amesema ziwa Victoria linanufaisha watu zaidi ya milioni 45 wa Afrika Mashariki hivyo ni muhimu kuhakikisha linahifadhiwa na kuendelezwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema kupanda miti ni kumbukumbu kubwa inayodumu hata aliyepanda anapokuwa hayupo.

Amewataka wananchi wote kuhakikisha wanaendelea kuotesha miti katika vyanzo vyote vya maji, makazi na maeneo mbalimbali kwasababu miti ni mazingira, mazingira salama ni maisha salama.

Zoezi la kuotesha miti limewashirikisha viongozi mbalimbali akiwamo Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Rose Ambrose ambaye amesisitiza umuhimu wa kuotesha miti katika vyanzo vya maji vyote nchini. Amesema Wizara ya Maji kupitia Bonde la Ziwa Victoria inakusudia kuotesha miti 10,000. Ambapo miti 6500 imeshaoteshwa. Aidha pamoja na miti 2000 iliyooteshwa, Wizara ya Maji inakusudia kuotesha miti 5000 katika maadhimisho ya siku ya Ziwa Victoria ambayo ni Mei 21.

Amesema chanzo cha maji cha Butimba ni muhimu kwa maisha ya wakazi wa Mwanza kwasababu chanzo hicho kinazalisha lita za maji kwa siku milioni 48 na kunufaisha zaidi ya wananchi 450,000. Lengo ni kukiendeleza ili kifikie uzalishaji wa maji lita milioni 96 ambazo zitakuwa zikinufaisha wakazi laki nane.

Naye Katibu Mtendaji Kamisheni ya Bonde la ziwa Victoria Dkt. Masinde Bwire amesema zoezi la kuotesha miti katika kutunza ziwa Victoria linafanyika kwa nchi zinazounda kamisheni hiyo zikiwemo Kenya, Uganda Burundi na Rwanda

Amesisitiza ushirikiano kwa kila mmoja ili kuhakikisha ziwa hilo linadumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.