Habari
*Wizara ya Maji kuwajengea uwezo wataalam kuhusu usalama wa mabwawa.*
Wizara ya Maji kwa kushirikiana na taasisi binafsi imeandaa mafunzo kuhusu usalama wa mabwawa Ili kuhakikisha mabwawa yanaendelea kuwa salama kwa matumizi yaliyokusudiwa hapa nchini.
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Wizara ya Maji Bw. Robet Sunday akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji katika mkutano na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano Wizara ya Maji Mtumba jijini Dodoma ametaja taasisi zinazoshirikiana na Wizara ya Maji kuwa ni Chemba ya Migodi Tanzania (CMT) na Kampuni ya Uhandisi ya City.
Mafunzo hayo yanatarajia kufanyika Jijini Mwanza kuanzia Oktoba 21 hadi 23, 2026 yakilenga kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wataalamu wa mabwawa ili kuhakikisha usanifu, ujenzi na uendelezaji wa mabwawa ya maji na mabwawa ya tope sumu yana viwango ili kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Washiriki wanaotarajiwa katika mafunzo ni kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakiwamo wamiliki wa mabwawa makubwa ya maji, wataalamu wa mabwawa waliosajiliwa, na wataalamu wanahusika na usimamizi wa mabwawa ya maji na tope sumu.
Mafunzo hayo yanabebwa na kaulimbiu "Usalama wa miundombinu ya mabwawa kuanzia kwenye hatua ya usanifu, utumiaji hadi ufungaji”.
Bw. Sunday ametumia fursa hiyo kuwaalika watunga sera, wataalamu na wamiliki wa mabwawa ya maji na tope sumu, taasisi na watu binafsi wanaojishughulisha na mabwawa pamoja na wadau wengine kujisajili kwenye mafunzo ya usalama wa mabwawa katika anuani; https://damsafetyconference.tz

